Mtoto wa simba aliwaongoza askari wa kulinda wanyama kwenda ulipo mwili wa mama yake ambaye alikuwa ameuawa katika mbuga moja ya kuhifadhi wanyama nchini India, kitendo ambacho maafisa wa wanyama pori wanakilelezea kuwa si cha kawaida.
Askari wa wanyama pori ambaye alimwona mtoto wa Simba akijificha vichakani, alimfuata na kugundua mwili wa Simba aliyeuawa katika kilima jirani.Uchunguzi uliofanyiwa mwili wa simba huyo ulibainisha kuwa alikufa katika mapigano na wanyama wengine huenda aliuawa na kundi la nyati.
Naibu mhifadhi wa Misitu katika eneo la Gir, Anshuman Sharma, amesema tabia ya simba huyo mtoto ni nadra kutokea na ni cha aina yake, kitu ambacho hajawahi kushuhudia katika miaka yake mingi ya kufuatilia tabia za simba.
Gir katika jimbo la Gujarat ni mahali wanapopatikana kwa wingi simba waAsia na kwa mujibu wa sense ya wanyama iliyofanyika mwaka 2010, kuna simba 411 katika mbuga hiyo.
"Jumamosi mchana, nilikuwa nafanya doria katika hifadhi ya Tulsi-Shyam nilipomwona mtoto wa simba akichificha katika vichaka,"mlinzi wa msitu Rana Mori ameiambia BBC.
''Watoto wa Simba huambatana na mama zao''
"Nilimfuatilia mtoto wa simba ambaye aliniongoza hadi kwenye mwili wa mama yake uliokuwa umelala katika kilima kidogo. Simba huyo jike aliitwa Rupa [likiwa na maana ya Mzuri].Kwanza alionekana kama aliyelala usingizi, lakini wakati hatikisiki, nilimsukuma na fimbo yangu. Ndipo nilipogundua kwamba simba huyo jike alikuwa amekufa," amesema.
Wakati Bwana Mori aliporejea na kundi la maafisa kuondoa mzoga huo, walimkuta mtoto huyo wa simba akiwa amekaa kando ya mwili wa mama yake.
Simba huyo jike ambaye alikuwa na umri wa miaka kumi na moja , alivunjika mbavu na kupata majereha ya ndani na kufa kutokana na kuvuja damu nyingi.
Mtaalam wa Simba Yadvendra Dev Jhala wa taasisi ya Wanyama Pori ya India ameiambia BBC kuwa hajawahi kusikia tukio kama hilo linalomhusu mtoto wa simba.
''Simba na walinzi wao''
Lakini amesema katika eneo la Gir hakuna mgogoro kati ya simba na binadamu na "kwa ujumla Simba wanawafahamu vizuri walinzi wao binafisi ".
Bwana Sharma anasema wanafahamika kwa tabia yao ya maisha ya kijamii: "Si kama Mbwa, hawatoi kucha au kutikisa mikia, lakini wanawatambua walinzi wanaowaona kila siku.."
Maafisa wa wanayama pori wanasema kwa ujumla watoto wa simba ni wategemezi mno wa mama zao kwa ajili ya maisha yao hadi wanapofikia umri wa miaka miwili na nusu hadi mitatu.
Mtoto huyo wa simba mwenye umri wa miezi 15, kwa sasa yuko chini ya uangalizi wa maafisa wa misitu.
"Mama yake, Rupa, alionekana kuwa mpweke na aliwinda peke yake,Lakini kwa sasa simba huyo jike ametoweka, tunatarajia mtoto huyo wa simba atajiunga na kundi lingine, au simba mwingine jike huenda akaanza kumtunza," amesema Bwana Sharma.
Source: BBC
0 comments:
Post a Comment