Facebook
Twitter

SOMA HADITHI KALI NA YA KUSISIMUA "SIMU YA AJABU "

SOMA HADITHI KALI NA YA KUSISIMUA "SIMU YA AJABU "
Fuatilia kisa hiki kila siku jioni kupitia ukurasa wa Simu ya Ajabu. Nawe waweza kutumiwa kisa hiki cha kusisimua kinachosomwa na wengi kupitia whatsapp namba 0713317171 au kuipiga namba hiyo

Wednesday, August 27, 2014

Namna ya Kuondokana na Tatizo la Kutojiamini


Kila kitu ambacho ni halisi kinawezekana. Bila shaka unakumbuka vizuri
kuhusu namna kutojiamini kwetu kunavyojengwa. Kwa kuwa tunajua chanzo,
ni rahisi kupata tiba.

Njia zifuatazo zinaweza kukusaidia katika kujenga kujiamini. Kuna njia nyingi
zinazopendekezwa, lakini kuna zile ambazo zimetumika sana katika kufanya
kazi hiyo. Hizi zifuatazo ni baadhi yake.

1. Yachunguze mawazo yako na vitendo vyako kwa uangalifu ili kujua ni kitu
gani hukufanya usisimke. Anza kufanya mambo ambayo unaona kwamba una
uwezo kuyafanya bila wasiwasi na kuchukua uamuzi unaojitegemea
kufuatana na utashi wako. Ikibidi unaweza kuomba msaada wa wengine,
lakini jaribu kila mara kufanya mambo kufuatana na unavyoyaona.
2. Jifunze kujithamini. inawezekana kwa miaka na miaka umekuwa unajiona
kama mtu usiye na thamani. Pia unaweza ukaona kwamba, hadhi uliyokuwa
nayo mbele ya ndugu, jumuiya na jamii imepungua. Jali ujuzi na vipaji vyako;
hata kama kuna ndugu wametajirika pamoja na kuwa ni mbumbumbu hiyo
isiwe chanzo cha kukuvunja nguvu. Iko siku utafanikiwa kama utaanza
kujiamini.
3. Jisamehe bila masharti yoyote. Kama maisha yako ya awali yalikuwa si ya
kiungwana, jisamehe na anza maisha yako upya. Njia bora ya kujisamehe ni
kujipenda bila masharti yoyote.
4. Pambana na hofu. Hofu ni kitu kibaya sana kwa sababu inaingilia kwenye
uwezo wako wa kufikiri. Ili ufanikishe malengo yako ya maisha huna budi
kuhakikisha kuwa huna hofu tena.
5. Fanya vitu unavyoviogopa. Orodhesha idadi ya vitu ambavyo ulikuwa
unaviogopa. Kisha anza na vitu ambavyo unaviogopa zaidi na jiulize kwa nini
usiweze kuvifanya.
6. Jifunze kupambana na kushindwa. Kubali kwamba kushindwa ni kama
chombo cha kujifunzia na si kitu cha kukukatisha tamaa. Jua, na amini
kwamba, bila kushindwa hakuna kukua. Pia elewa kwamba, kushindwa siyo
dalili ya udhaifu, bali uimara.
7. Kubali kupingwa kwa moyo mkunjufu. Watu wa nje wanaweza kukusaidia
kwa mambo yako mengi ambayo huyaoni. Watu wakikusoa, hata kama ni
kifedhuli, chukua yaliyo mema na yafanyie kazi.
8. Fanya mazoezi ya kujiamini. Jifunze kusimama kwa miguu yako mwenyewe
kimawazo, kiimani na kimatendo. Bila kuonyesha ujeuri unaweza kulinda haki
zako, matarajio yako na maadili yako. Anza kujifunza kujenga taswira ya
kujiona uko mwenyewe na unamudu kila kitu. Bila msaada na utegemezi kwa
wengine.
9. Jipongeze kwa maneno mazuri. Jiamini na daima jipe moyo kwa maneno
ambayo yatakutia moyo ili kwenda vyema katika shughuli zako. Usitumia
maneno ya kejeli, kashfa na chuki dhidi yako mwenyewe, ‘mimi ni mjinga kweli
yaani jambo dogo kama hili limenishinda….’ Unaweza kujisemea baada ya
kukosea. Kama umekosea, jiambie maneno mazuri ya kujipa moyo na siyo
maneno ya kero na fadhaa.
10. Usijilinganishe na wengine, bali iga. Kama wengine wanakuzidi
isikukatishe tamaa ila iwe ni chachu ya maendeleo . jiambie, ‘kama
wanaweza, maana yake ni kwamba, inawezekana, nami nitaweza tu.’
11. Fikiria mambo ambayo yanakufanya usiwe na furaha na jaribu kupambana
nayo na kuondokana nayo. Kila wakati jiulize, ni kwa nini uko kwenye hali ya
kihisia uliyo nayo. Usikubali kufuga huzuni kwa muda mrefu ndani mwako.
12. Fanya mambo uyapendayo zaidi. Kujiamini kutaongezeka kama utafanya
mambo unayoyafahamu zaidi kwa sababu ni rahisi kuyafanikisha na kukuletea
furaha.
13. Jifunze namna ya kushughulikia hasira zako. Mtu asiyejiamini ana
kawaida ya kutaka kupendwa na watu, na katika kufanya hivyo, hapendi
kuonekana kuwa ni mtu mwenye hasira na hivyo kuendelea kubakia na hasira
zake moyoni hata kama ameudhiwa.
14. Kuzuia hasira hakusaidii, zaidi ya kukuongezea kuchanganyikiwa na
kukufanya kuwa mtu usiye na furaha au kisirani. Ukiudhiwa, mwambie
aliyekuudhi kinaganaga, lakini katika mazingira ya kistaarabu ambayo
hayawezi kukuumiza wewe wala mtu ambaye amekuudhi.

0 comments:

Post a Comment


  • Copyright 2014 Uvunguni